Je wazijua Bahari Mbili Zinazokutana Lakini Maji 'Hayachanganyikani'?
UMEONA picha
na video zinazosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii zikionesha
mahali ambapo bahari mbili zinakutana lakini bado maji yake yanaonekana
kutochanganyika?
Kama
hujaona basi kwa taarifa yako, bahari mbili za Atlantic na Pacific,
kuna sehemu zinakutana lakini cha ajabu, maji yanaonekana
‘kutochanganyika’, upo mpaka kabisa katika maji, unaoyatofautisha maji
ya bahari moja na bahari nyingine, ya upande mmoja yakionesha kuwa na
rangi tofauti na ya upande wa pili.
Wengine
wanalihusisha tukio hili na nguvu zisizoonekana, wengine wanaeleza ni
miongoni mwa ishara kwamba Mungu yupo na wengine hawaelewi chochote.
Lakini nini hasa kinachosababisha hali hii?
Kuweka
mambo sawa, lazima ieleweke kwamba si kwamba maji ya bahari hizo mbili
hayachanganyikani, isipokuwa huchukua muda fulani kuchanganyikana. Kwa
sababu gani?
Pacific
ndiyo bahari kubwa kuliko zote duniani, ikikusanya maji kutoka
Antarctica mpaka Arctic, kuanzia ncha ya Kaskazini mpaka ncha ya Kusini
ya dunia. Kwa kuwa sehemu kubwa ya vyanzo vya maji yake ni theluji,
kiwango cha chumvi kwenye maji ya bahari hiyo, ni kidogo ukilinganisha
na maji ya bahari ya Atlantic.
Kisayansi,
maji yenye kiwango tofauti cha chumvi, huchukua muda mrefu
kuchanganyikana, na ushahidi wa hili, inaelezwa kwamba eneo ambalo mto
Amazon unaingiza maji baharini, kwa kuwa maji ya mto hayana chumvi
tofauti na ya baharini, ukiwa umbali wa zaidi ya mita 200 baharini,
usawa wa eneo hilo, kuna maji baridi yasiyo na chumvi kabisa.
Kwa
hiyo, sababu ya kwanza ya kitaalamu ya maji hayo ‘kutochanganyikana’,
ni tofauti ya kiwango cha chumvi kati ya bahari hizo mbili, Atlantic
ikitajwa kuwa ndiyo yenye chumvi nyingi zaidi.
Sababu
nyingine, inaelezwa kwamba kitaalamu, maji ya Bahari ya Atlantic,
yanajongea kuelekea upande wa Kusini. Wakati huohuo, maji ya Pacific,
yenyewe yanajongea kwa mfumo ambao kitaalamu huitwa circumpolar
movement, yaani mwendo wa kuzunguka kutoka ncha moja ya dunia mpaka
nyingine.
Kwa
lugha nyepesi, maji ya Pacific, yanajongea kwa mfumo wa kuzunguka duara
lakini yakitokea Mashariki. Mkondo wa Bahari ya Atlantic una nguvu
zaidi kwa sababu una uelekeo mmoja, kwa hiyo katika eneo yanapokutana,
maji ya Atlantic yanakuwa kwenye kasi tofauti inayokinzana na maji ya
Pacific, kwa hiyo yanalazimika kusafiri kwenye mstari mmoja ulionyooka
kwa umbali fulani kabla ya baadaye kuanza kuchanganyikana.
Sababu
ya tatu, inaelezwa kwamba kasi ya maji ya juu ya bahari, ni tofauti na
kasi ya maji ya chini ya bahari, kwa hiyo pale bahari hizo mbili
zinapokutana, maji yanayoanza kuchanganyikana, huwa ni ya chini kwa
sababu ya kasi yake kisha baadaye, ndiyo maji ya juu nayo
huchanginyakana taratibu kwa sababu ya kasi yake.
Kwa
hiyo, ile dhana kwamba bahari hizo mbili hazichanganyikani, si ya kweli
kwa sababu kitaalamu imethibitika kwamba maji hayo huchanganyikana.
Comments