KUSILAWE: Nitahakikisha CCM inashinda majimbo yote Dar
Mkoa wa Dar es Salaam. Katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, anasema, “Nitapiga mzigo hadi nihakikishe CCM Dar inarejesha majimbo na kata zote zilizokwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015.”
Kusilawe pia alitoa ahadi hiyo hivi karibuni mbele ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulembo katika ziara aliyoifanya mkoani Dar es Salaam kuimarisha chama.
Alisema, “Nikikumbuka yaliyotokea Dar es Salaam katika uchaguzi uliopita, ninakosa raha. Siamini kilichotokea Dar na ndiyo maana tunazidi kujipanga.” Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam ilishinda majimbo manne na kupoteza majimbo sita.
Majimbo ambayo CCM ilishinda na wabunge wake katika mabano ni Kigamboni (Dk Faustine Ndugulile), Ilala (Mussa Zungu), Mbagala (Issa Mangungu) na Jimbo la Segerea (Bonnah Kaluwa).
Anapozungumzia matokeo ya uchaguzi huo katika kata anasema, “Jimboni Ubungo, CCM tulipata kata mbili, Kinondoni kati ya kata 13, tulipata 6, Segerea kata zote zipo upinzani na hata Ilala upinzani una kata nyingi. Ndiyo maana kila ninapokumbuka hayo, nakosa raha.” Hata hivyo, anasema hali ya sasa na namna chama chake kinavyojiandaa mapema, hana wasiwasi na chama kinausubiri uchaguzi huo.
“Unajua kwa sasa, hakuna muujiza wa kuifanya CCM ipoteze viti tena kama ilivyotokea mwaka juzi.” Anapotakiwa kufafanua kauli yake, Kusilawe alisema, “Mpaka sasa Serikali ya chama Tawala imefanya na inaendelea kufanya kazi kubwa na nzuri kwa Watanzania na kila Mtanzania anaiona, anaikubali na kuifurahia.
We unadhani watu wa Dar es Salaam hawana macho ya kuona utumishi huu wa Serikali ya Awamu ya Tano namna unavyowanufaisha!” “Kinachofanywa na kuonekana, kinaonesha kabisa kazi zote bora zimefanywa na serikali ya CCM na hao wengine wamebaki tu kama wasanii,” anasema na kuongeza, “Ndiyo maana wengi ambako CCM haipo madarakani walidhani baada ya uchaguzi hali itakuwa nzuri, lakini sasa wanaona katika maeneo yao hali inakuwa mbaya zaidi.
Naamini wamejifunza na katika chaguzi zijazo, hawatarudia kosa.” Kuhusu mbinu atakazotumia kwa ushirikiano na wanachama na viongozi wenzake mkoani Dar es Salaam, Kusilawe anasema: “Tutahakikisha Serikali inatekeleza kikamilifu Ilani yake na kutimiza ahadi zake kwa kuwaondolea kero wananchi.
“Njia nyingine tutakayotumia ni kuisimamia zaidi Serikali iendelee kutenda na kutoa haki kwa kila mwananchi kupitia upatikanaji wa huduma za kujamii kuwa bora, za kutosha, kwa wakati na kuzifanya kuwa endelevu huku watendaji wote wabovu wanapobainika, wawekwa pembeni kwa hatua zaidi za kisheria. Kwa hili, nashukuru Rais John Magufuli anaendelea kwa kuzingatia ukweli na haki; na watu wanaona na kufurahi,” alisema.
Anasema kwa msingi huo, CCM mkoani Dar es Salaam inataka viongozi wote wa Serikali wafanye kama anavyofanya Rais Magufuli kwa kutumia wananchi kwa dhati, bila ubaguzi wala upendeleo.
Kusilawe anasema, “Changamoto kama miundombinu duni ya umeme, maji katika huduma nyingine za kijamii zizidi kuboreshwa na kupatikana kwa wakati kwa watu wote kama juhudi hizo zinavyoendelea kufanyika sasa,” .
Njia nyingine aliyoiita silaha ya ukombozi wa kata na majimbo ambayo chama tawala hicho kilipoteza katika Uchaguzi Mkuu uliopita, anasema ni kuendelea kuwajibika na kuwakumbusha Watanzania mambo mema yanayofanywa na serikali yao.
Kiongozi huyo wa CCM aliyeanza kutumikia wadhifa huo mkoani Dar es Salaam Aprili 13, mwaka huu anasema, siri kubwa ya mafanikio katika malengo hayo ni kuhakikisha watu wanaondokana na sintofahamu ya kutojua kazi njema zinazofanywa na Serikali yao.
“Lazima watu wajue serikali yao inafanya nini. Hii ni pamoja na kuondoa sintofahamu kwa makundi ya wafanyakazi, wajasiriamali, wakulima, vijana na akina mama ili kwamba, hao wakielewa na kutuunga mkono, tutavuka salmaa chaguzi zijazo.
Tuna uhakika huo maana hao watu wote wanategemeana,” anasema. Akaongeza, “Ninavyowafahamu Watanzania na hasa watu wa Dar es Salaam, uchaguzi ujao tutashinda sana maana Watanzania wameona na kijufunza njia sahihi ili wafikie maendeleo wanayokusudia.
Naamini kabisa kila kura ikipigwa na kuhesabiwa kwa haki,CCM Dar tutashinda kwa kishindo kikubwa.” Anasema alipokwenda mkoani Shinyanga mwaka 2015 na kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa akitokea Mtwara Mjini alipokuwa Katibu wa CCM wa Wilaya kati ya Mwaka 2014 na 2015, alikuta mkoa wa Shinyanga ukiwa na majimbo yote katika mikono CCM, lakini kata 32 kati ya kata 100 zilikuwa za upinzani hadi zilipoongezwa na kufikia kata 126 wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
“Tulijipanga na wenzangu tukachambua na kuwaeleza wananchi namna ilani ya CCM ilivyotekelezwa tangu mwaka 2010 na tukaangalia ilikuwaje, yapi yametekelezwa na yapi bado, sababu na mipango iliyopo; tukawaelimisha wananchi wakatuelewa na kutuamini.”
Anasema, “Matokeo yake, tulifanikiwa kushika majimbo yote, licha ya baadhi ya viongozi na wanachama kuhama na kati ya kata 32 zilizkuwa upinzani, tukashinda kata 23 na kuzirudisha CCM.”
Comments