Ujenzi viwanda vipya, kufufua vya zamani kuimarishwa
UJENZI wa msingi wa viwanda ikiwamo kuendeleza viwanda vipya na kufufua vya zamani, pamoja na kupanua ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2017/18. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, miradi mingi utekelezaji wake ulianza mwaka 2016/17 hivyo inaendelea. Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, kuhuisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) hususan kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege nne, miradi ya chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma. Mingine ni uanzishwaji/uendelezaji wa kanda maalumu za kiuchumi, mtambo wa kuchakata gesi asilia Lindi, na shamba la kilimo na uzalishaji sukari Mkulazi. Akizungumzia ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, alisema itahusisha miradi ya uendelezaji wa eneo la viwanda Tamco Kibaha, tathmini ya matumizi ya eneo la kiwanda cha Gene...