Wachezaji wa kigeni Yanga, Simba wazua zogo bungeni
Hata hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dk Harrison Mwakyembe aliliambia Bunge kuwa madai hayo si ya kweli kwani wachezaji wa kigeni walioshiriki ligi hiyo ni 35 tu. Baadhi ya wachezaji wa kigeni walioko Yanga ni Thaban Kamusoko (Zimbabwe), Obrien Chirwa (Malawi), Haruna Niyonzima (Rwanda), Vincent Bossou (Togo).
Wachezaji wa kigeni walio Simba ni Besela Bukungu (Congo DRC), James Kotey(Ghana), Juuko Murshi (Uganda), Laudit Mavugo (Burundi), James Abiey (Ghana). Wachezaji hao walisababisha wabunge kuhoji kama uwepo wao una athari kwa kiwango cha soka la wachezaji wazawa.
Waziri Mwakyembe alilieleza Bunge kuwa kati ya wachezaji 112 ambazo timu za Ligi Kuu ya Vodacom ziliruhusiwa kusajili ili kucheza ligi hiyo, 35 ndiyo wageni idadi ambayo ni ndogo kwa timu 16 zinazoweza kusajili wachezaji 30. Waziri Mwakyembe alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM).
Alisema wachezaji hao walikuwa asilimia saba tu ya wachezaji wote walioshiriki ligi hiyo hivyo hawajachangia kushusha kiwango cha soka kama inavyohofiwa. Dk Mwakyembe alisema, kuongezeka kwa wachezaji wa kigeni hakuna athari katika soka kwani mwaka 2010/15 walikuwa watano na baadaye wakaongezwa hadi kufikia wachezaji saba kila timu.
“Kenya ilipunguza kutoka wachezaji saba hadi wachezaji watano,” alisema. Alisema uwepo wa wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya Tanzania umeongeza ushindani kati ya wachezaji,weledi na nidhamu na kuchochea vilabu kupanua wigo wao wa mapato katika usajili.
Alisema,kuchanganya wachezaji wazawa na wageni ni fursa ya pekee kwa wachezaji wetu kujifunza kutoka kwa wenzao na husaidia kutangaza ligi yetu nje na wao kufuatiliwa zaidi na timu zao za Taifa.
Dk Mwakyembe alisema hata hivyo katika ligi hiyo, timu zisizo na wachezaji wa kigeni zilifanya vizuri ikiwamo Kagera Sugar iliyoshika nafasi ya tatu na Mtibwa Sugar iliyoshika nafasi ya tano.
Alisema hata wachezaji bora wa mwaka huu, Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na Simon Msuva wa Yanga hawakutoka timu zenye wachezaji wengi wa kigeni nchini. Alisema wachezaji wa kigeni hawana athari katika ligi hiyo kutokana na ukweli kwamba ni wachezaji wachache tu wa nje wanaoshiriki katika ligi hiyo.
Alisema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mwamoto aliyetaka kujua sababu za kuongezeka au kupungua wachezaji hao ni nini na manufaa yake. Dk Mwakyembe alisema kwa mujibu wa taratibu za usajili za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wachezaji wa nje wanaoruhusiwa kucheza kwenye ligi Kuu ya Tanzania ni saba kwa kila klabu.
“Tulianza na wachezaji watano kati ya mwaka 2010 hadi 2015 na kuanzia musimu wa 2015/16 idadi imeongezeka hadi saba. Alisema wachezaji wa nje kwenye Ligi Kuu ya Tanzania wanaongezeka kufuatia maombi ya wadau wa soka hasa kubwa za Simba na Yanga zenye uwezo wa kulipa mishahara minono kwa wachezaji hao.
Comments