Mdee, Bulaya Wasimamishwa Kuhudhuria vikao vya Bunge Hadi Mwaka 2018
DODOMA:
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya wote
wa CHADEMA wameadhibiwa kwa kusimamishwa na Bunge kuhudhuria vikao
vyote vilivyosalia vya mkutano wa 7 wa Bunge la Bajeti linaloendelea
hivi sasa mjini hapa, pia hawatohudhuria mkutano wa 8 na wa 9 kwa utovu
wa nidhamu.
Aidha Bunge limeamua kuwa, wabunge hao watarudi kuhudhuria vikao kuanzia kwenye Bunge la Bajeti la mwaka ujao (2018).
Tukio
hilo limeibuka kufuatia vurugu zilizoibuka Ijumaa iliyopita baada ya
Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde kudai kwamba wapinzani bungeni
humo wanatetea wezi wa mchanga wa dhahabu, hali iliyosababisha Mbunge wa
Kibamba, John Mnyika kuibuka na kubishana. Mbunge mwingine ambaye
hakujulikana jina lake aliwasha maiki na kumuita Mnyika mwizi, Mnyika
alikitaka kiti cha Spika kimuamuru mbunge huyo kufuta kauli yake lakini
spika alisema hakumsikia aliyesema maneno hayo.
Baada
ya mabishano kati ya Spika na Mnyika, spika aliamuru Mnyika atolewe nje
na polisi wa Bunge, hali iliyosababisha Halima Mdee na Ester Bulaya,
waiingilie kati kuwazuia askari hao kumtoa nje. Jambo hilo lilisababisha
tafrani licha ya Mnyika kutolewa nje huku wabunge wa upinzani wakitoka
nje.
Spika
alitangaza kumsimamisha Mnyika asihudhurie vikao vya bunge kwa wiki
moja huku Ester Bulaya na Halima Mdee akisema wataandikiwa barua ili
wakahojiwe na Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge ambapo leo wameadhibiwa
wasihudhurie vikao vya bunge kama ilivyoelezwa hapo mwanzo.
Comments