Hans Poppe: Simba kaeni mkao wa kula usajili
Simba imepanga kusajili wachezaji sita wapya kuimarisha kikosi chake kitakachoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) na Ligi Kuu Vodacom. Hans Poppe alisema jana, mazungumzo na nyota hao yanakwenda vizuri na kilichobaki ni kukamilisha makubaliano ya mishahara huku wakisubiri dirisha la usajili kufunguliwa ili wawasilishe majina Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Unajua dirisha la usajili halijafunguliwa. Kinachofanyika hivi sasa ni mazungumzo ya makubaliano na ikiwezekana kusaini mkataba wa awali ili wakati dirisha likifunguliwa, iwe kazi rahisi kukamilisha taratibu nyingine,” alisema.
Hata hivyo, Poppe alikataa kuwataja wachezaji hao kwa madai hawajakamilisha taratibu za usajili na wanahofia wasichukuliwe na Yanga. Pamoja na kukataa kuwataja, baadhi ya wachezaji wanaohusishwa kuhamia Simba ni Shomari Kapombe na Aishi Manula (Azam).
Wengine ni Mbaraka Yusuf (Kagera Sugar), Salum Kimenya (Prisons ya Mbeya). Alisema mikakati yao ni kukamilisha usajili wao mapema na taratibu zote zinazotakiwa ili kupata muda mzuri wa maandalizi ya ligi.
Simba imepania kutwaa taji hilo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara linaloshikiliwa na Yanga kwa misimu mitatu mfululizo huku wakionekana kama wasindikizaji kwa kipindi chote hicho.
Comments