JPM, marais EAC wapongeza Uhuru

RAIS John Magufuli amewaongoza marais wengine wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kumpongeza Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kuibuka mshindi wa kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumanne wiki hii, Rais Magufuli alituma salamu hizo za pongezi kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema; “Nakupongeza Ndugu Uhuru Kenyatta kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Kenya kwa kipindi kingine.

Nakutakia mafanikio mema.” Wengine waliotuma salamu zao ni Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda na Pierre Nkurunziza wa Burundi. Waangalizi `wafagilia’ Wakati aliyekuwa mpinzani wake katika kinyang’anyiro hicho cha urais, Raila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na kambi yake ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA) wakilia kwa kile wanachodai kuchezewa rafu katika uchaguzi huo, waangalizi wa kimataifa kwa umoja wao wameeleza kufurahishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, huku wakisema matokeo ya kura zilizotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinafanana kabisa na zile walizonazo.

Waangalizi hao kupitia kundi la ELOG wamesema walizungukia vituo 1,692 kati ya 40,000 vilivyokuwa zimetangazwa na IEBC. Pia matokeo ya kwenye Fomu 34A, yameonekana kushabihiana pia, hivyo kuonesha kwamba hakukuwa na udanganyifu uliofanyika.

Maaskofu, Makanisa wasisitiza umoja, mshikamano Katika hatua nyingine, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya (KCCB) limesema baada ya uchaguzi kumalizika Rais Kenyatta ana jukumu kubwa la kuhakikisha anawaunganisha Wakenya. Aidha, baraza hilo limewataka wanasiasa kuwa makini na kauli zao kwa kuhakikisha haziwezi kuleta mtafaruku utakaosababisha uvunjifu wa amani bali kuendeleza amani miongoni mwa jamii.

“Tumepokea taarifa za kuwepo kwa vifo vya watu, lakini hakuna uhai wa mtu utakaopotea kwa sababu ya uchaguzi, kwa maana uchaguzi umekwisha.” Baraza hilo pia limetaka kuwepo kwa utulivu miongoni mwa wananchi baada ya shughuli za upigaji kura kumalizika. Wakati huohuo, Baraza la Makanisa Kenya (NCCK) limewataka viongozi wa kisiasa kuzungumza na wafuasi wao ili kupunguza taharuki iliyoibuka katika maeneo mbalimbali ya nchini humo.

Aidha, limeitaka polisi kuacha kutumia nguvu na risasi kuwazuia wafuasi wa vyama vya siasa hasa vile vya upinzani. Pia wametaka viongozi hao, kuendelea kuzungumza juu ya umoja wa Kenya. Mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha KTN, Duncan Kihemba alikamatwa wakati akichukua matukio ya waandamanaji katika eneo la Kibera. Mwanahabari huyo alikamatwa kwa kuvalia mavazi ya polisi ya kuzuia risasi bila kuwa na kibali kutoka kwa jeshi la polisi nchini humo.

Hata hivyo, furaha ya wafuasi wa Rais mteule, Uhuru waliomwagika mitaani kusherehekea kuibuka kwake kuwa mshindi, iliingia dosari baada ya watatu kati yao kufa katika ajali za barabarani. Aidha, wananchi wenye hasira, walichoma magari karibu na makazi ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi usiku na Chebukati, Uhuru aliyezaliwa na kukulia Ikulu ya Kenya kutokana na baba yake, Jomo Kenyatta kuwa Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, alipata kura 8,203,290, sawa na asilimia 54.27 ya kura zote 15,0673,662 (asilimia 78.91 ya watu milioni 19.6 waliojiandikisha), wakati mshindani wake, Raila aliyesusia matokeo akidai kuchezewa rafu, alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.

Wengine waliojitokeza kutaka kuiongoza Kenya, lakini kura zao hazikutosha ni Joseph Nyaga (42,259), Abduba Dida (38,093), Dk Ekuru Aukot (27,311), Japheth Kaluyu (16,482), Profesa Michael Wainaina (13,257) na Cyrus Jirongo (11,705).

Ajali barabarani, moto Katika tukio la vifo vilivyotokana na ajali, kwa mujibu wa taarifa za Polisi, waendesha pikipiki wawili waliokuwa wanasherehekea ushindi huo mara baada ya Chebukati kuhitimisha kusoma matokeo ya uchaguzi, walifikwa na mauti katika eneo la Magumu katika Jimbo la Kinangop.

Aidha, mtu mwingine alikufa baada ya kugonjwa na lori katika mji wa Molo ambako mamia ya wafuasi wa Uhuru na chama chake cha Jubilee, walikuwa wameingia barabarani kusherehekea ushindi huo dhidi ya wagombea urais wengine saba, akiwamo mshindani wake mkubwa, Raila Odinga.

Wakati watu hao waliaga dunia kutokana na ajali, makazi ya Chebukati yalinusurika kuchomwa moto na watu wasiojulikana, lakini majirani zake wakiathirika kutokana na magari yao kuteketezwa.
Waliochoma moto walifanya hivyo muda mfupi baada ya Chebukati kumaliza kusoma matokeo ya uchaguzi mkuu uliomrejesha Uhuru madarakani. Imeelezwa kuwa, moto huo ulichomwa karibu na makazi ya mwenyekiti huyo wa IEBC yaliyoko katika shamba lake la Saboti huko Kiminini, Kaunti ya Trans Nzoia.
Hata hivyo, nyumba yake haikuathiriwa na moto huo, ingawa haukuwa mbali na makazi hayo. Kutokana na matokeo hao, imeelezwa makundi kadhaa ya wapinga matokeo walifanya vurugu katika maeneo kadhaa, yakiwemo katika mji wa Kisumu na maeneo ya Kibera na Mathare, jijini Nairobi.

Hata hivyo, polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama, Fred Matiang’i ameonya juu ya vurugu hizo, akisema jeshi la Polisi halitawaacha salama wote watakaojihusisha na matukio yanayotishia uvunjifu wa amani.

Wanasiasa nchini wapongeza Katika hatua nyingine wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, wamepongeza hatua ya Kenya kumaliza uchaguzi salama huku wakitaka nchi hiyo kuhakikisha inaendelea kulinda amani iliyopo ili kutoleta vurugu zitakazoweza kusababisha maafa.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu uchaguzi huo wa Kenya, Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema, Wakenya wamefanya uchaguzi vizuri inagawa kulikuwepo na changamoto mbalimbali.
Alisema licha ya uchaguzi huo kufanyika vizuri lakini changamoto za teknolojia na hasa suala la udukuzi linaweza kufanyiwa kazi na hata nchi nyingine ikiwemo Tanzania zinaweza kujifunza kupitia changamoto hiyo.
“Hata sisi huku bila kusemea upande wowote. Jambo kubwa ni kuonesha kuwa matokeo ni ya kuaminiwa, na si tena kuwepo na matokeo ambayo yanakuwa na mashaka ndani yake,” alisema Profesa Baregu.

Aliongeza kuwa kwa sasa serikali inatakiwa kufuatilia kama hakuna matukio yanayotishia usalama wa nchi hiyo, na kwamba hawatakiwi kujisahau na kujikuta wakiingia tena katika machafuko kama ya miaka ya nyuma ambayo yameacha makovu hadi leo.

Kuapishwa Haijatangazwa siku ya kuapishwa kwa Uhuru, Rais wa nne wa Kenya baada ya Mzee Kenyatta, Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki, lakini kwa mujibu wa taratibu, Rais anapaswa kuapishwa siku 14 baada ya kutangazwa kuwa mshindi, na endapo kutakuwa hakuna pingamizi la kisheria kortini.

Maoni yenu wadau kuhusu hii

Comments

Popular posts from this blog

Diamond atangaza kufunga ndoa mwaka huu